| Chapter 2 |
1 | Siku ya tatu kulikuwa na arusi mjini Kana, mkoani Galilaya. Mama yake Yesu alikuwapo,
|
2 | naye Yesu alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake.
|
3 | Divai ilipokwisha, mama yake akamwambia, "Hawana divai!"
|
4 | Yesu akamjibu, "Mama, usiniambie la kufanya. Saa yangu bado."
|
5 | Hapo mama yake akawaambia watumishi, "Lolote atakalowaambieni, fanyeni."
|
6 | Hapo palikuwa na mitungi sita ya mawe, ambayo kila mmoja uliweza kuchukua kiasi cha madebe mawili au matatu. Ilikuwa imewekwa hapo kufuatana na desturi ya Kiyahudi ya kutawadha.
|
7 | Yesu akawaambia, "Ijazeni mitungi hiyo maji." Nao wakaijaza mpaka juu.
|
8 | Kisha akawaambia, "Sasa choteni mkampelekee mkuu wa karamu."
|
9 | Mkuu wa karamu alipoonja hayo maji, kumbe yalikuwa yamegeuka kuwa divai. Yeye hakujua ilikotoka, (lakini wale watumishi waliochota maji walijua). Mkuu wa karamu akamwita bwana arusi,
|
10 | akamwambia, "Kila mtu huandaa divai nzuri kwanza hata wakisha tosheka huandaa ile hafifu. Lakini wewe umeiweka divai nzuri mpaka sasa!"
|
11 | Yesu alifanya ishara hii ya kwanza huko Kana, Galilaya, akaonyesha utukufu wake; nao wanafunzi wake wakamwamini.
|
12 | Baada ya hayo, Yesu alishuka pamoja na mama yake, ndugu zake na wanafunzi wake, wakaenda Kafarnaumu ambako walikaa kwa siku chache.
|
13 | Sikukuu ya Wayahudi ya Pasaka ilikuwa imekaribia; hivyo Yesu akaenda Yerusalemu.
|
14 | Hekaluni aliwakuta watu wakiuza ng`ombe, kondoo na njiwa, na wavunja fedha walikuwa wamekaa kwenye meza zao.
|
15 | Akatengeneza mjeledi wa kamba, akawafukuza wote nje ya Hekalu pamoja na kondoo na ng`ombe wao, akazimwaga sarafu za wenye kuvunja fedha na kupindua meza zao.
|
16 | Akawaambia wale waliokuwa wanauza njiwa, "Ondoeni vitu hivi hapa. Msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa soko!"
|
17 | Wanafunzi wake wakakumbuka kwamba Maandiko yasema: "Upendo wangu kwa nyumba yako waniua."
|
18 | Baadhi ya Wayahudi wakamwuliza Yesu, "Utafanya muujiza gani kuonyesha kwamba unayo haki kufanya mambo haya?"
|
19 | Yesu akawaambia, "Vunjeni Hekalu hili, nami nitalijenga kwa siku tatu."
|
20 | Hapo Wayahudi wakasema, "Hekalu hili lilijengwa kwa muda wa miaka arobaini na sita. Je, wewe utalijenga kwa siku tatu?"
|
21 | Lakini Yesu alikuwa anaongea juu ya Hekalu ambalo ni mwili wake.
|
22 | Basi, alipofufuliwa kutoka wafu, wanafunzi wake walikumbuka kwamba alikuwa amesema hayo, wakaamini Maandiko Matakatifu na yale maneno aliyokuwa akisema Yesu.
|
23 | Yesu alipokuwa Yerusalemu kwa sikukuu ya Pasaka, watu wengi walimwamini walipoona ishara alizozifanya.
|
24 | Lakini Yesu hakuwa na imani nao kwa sababu aliwajua wote.
|
25 | Hakuhitaji kuambiwa chochote juu ya watu, maana aliyajua barabara mambo yote yaliyomo mioyoni mwao.
|